Wenyeviti takribani 30 wa vitongoji vinavyounda Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mugumu wameibana Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti mkoani Mara iwalipe malimbikizo ya posho zao za vikao na madaraka, kiasi cha Shilingi milioni 26, ambayo ni malimbikizo ya kuanzia mwaka 2019 hadi 2024 kwa mujibu wa wenyeviti hao.
Walitoa malalamiko hayo wakati wa kikao cha kawaida cha Baraza la Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mugumu kilichofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri hiyo hivi karibuni.
“Watulipe posho zetu ni haki zetu za msingi sio hisani,” alisema Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nyamerama, Mwita Marwa Nyanswi.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Bwenda Ismail Bainga, alikiri kuwepo kwa madai ya posho za wenyeviti hao.